National News

MAKONDA NA RABIA WAKUTANA NA DANIEL CHONGOLO OFISINI KWAKE

Tarehe: 27 Oct, 2023


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka wateule katika Chama hicho kuanza rasmi majukumu yao wakitambua imani kubwa waliyopewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, chini ya Mwenyekiti wa CCM Samia Suluhu Hassan, kutumikia chama kupitia nafasi hizo walizoteuliwa.

Amesema hayo alipokutana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda, na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, walipofika ofisini kwake, ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuonana naye, kujitambulisha na kuanza kazi, baada ya kukabidhiwa ofisi zao rasmi na watangulizi wao.

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Chongolo amesema kuwa nafasi hizo mbili, Idara ya Itikadi na Uenezi na Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati ya CCM, hivyo wanapaswa kujua kuteuliwa kwao ni sehemu ya kuongeza chachu na kasi ya idara hizo kutekeleza malengo yaliyokusudiwa na CCM, katika kutumikia wananchi na kuzisimamia Serikali zote mbili za CCM.

“Karibuni sana, hongereni sana kwa kuaminiwa na kuteuliwa, ujio wenu utakuwa sehemu ya kuongeza kasi ya yale ambayo chama tumekusudia, uenezi na siasa ndiyo kila kitu, mmeaminiwa na kuteuliwa kushika maeneo muhimu,” amesema Chongolo.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab