National News

WAZIRI MAJALIWA AWATAKA WADAU WA MADINI KUTUMIA TEKNOLOJIA

Tarehe: 26 Oct, 2023


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa madini wajielekeze katika kutumia teknolojia za kisasa katika uchimbaji madini ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na uchimbaji usio endelevu.
 
Ameyasema hayo leo  Oktoba 26, 2023 katika Hafla ya Kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIF) wa mwaka 2023. Waziri Mkuu amefunga mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
 
Waziri mkuu Majaliwa amewataka wadau hao waweke mikakati ya kuimarisha kaguzi katika masuala ya afya, usalama na utunzaji wa mazingira dhidi ya uharibifu unaoweza kuepukika katika shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
 
Pia, Waziri Mkuu amesisitiza wadau mbalimbali waunganishwe na kuweka mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini kwa kufanya tafiti za madini mkakati, madini ya viwanda na madini ya metali.
 
Aidha Majaliwa amesema kutokana na uwekezaji katika Sekta ya Madini kuhitaji mitaji mikubwa, hivyo ametoa rai kwa taasisi za kifedha kuweka mazingira nafuu ya taarifa za kutoa mitaji ya kuendeleza miradi ya madini.
 
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wadau wa madini waendelee kuunga mkono juhudi za dhati za Serikali ili kuiwezesha Sekta ya Madini kukua na kutoa mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.
 
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau hao wa sekta hiyo kuwa, Serikali itazingatia ushauri na mapendekezo yaliyotolewa ili kuendelea kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab