RC KIGOMA AMWAGIZA DC WA UVINZA KUUNDA TUME KUTATHMINI MATUMIZI YA SH. MILIONI 500 ZA UJENZI KITUO CHA AFYA
Tarehe: 21 Oct, 2023
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinnah Mathamani kuunda tume itakayofanya Tathmini ya matumizi ya Fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Rukoma kilichopo Wilayani humo kufuatia fedha hizo kumalizika kabla ya mradi huo kukamilika.
Maelekezo hayo ameyatoa wakati akikagua miradi ya maendeleo katika kata za Mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Uvinza, ambapo ameonesha kutoridhishwa kutokana na kazi zilizofanyika katika ujenzi huo kutolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa kutekeleza mradi.
"Sikubaliani na sababu zilizotolewa na watendaji wanaohusika na usimamizi wa mradi ikiwemo suala la kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi na kusababisha kutokamilika kwa Kituo hicho huku maeneo mengine yakikamilisha miradi kama hiyo kwa kiasi kama hicho cha fedha" amesema.
"Haiwezekani ishindikane hapa Rukoma wakati maeneo mengine imewezekana, nataka wataalam waje wafanye tathmini na kuona uhalali wa matumizi ya fedha na thamani halisi kama imefikiwa kwani kuna kila dalili ya ubadhilifu wa fedha za Umma hapa" amesema Andengenye.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza kutafuta fedha kutoka mapato ya ndani ili kumalizia ujenzi wa kituo hicho na kukiwezesha kutoa huduma za Afya kwa wananchi mara baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewahimiza watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa kwani Serikali imewaamini kusimamia kazi wanazopewa kwa lengo kusuma gurudumu la maendeleo ya nchi.