National News

RC KIGOMA AAGIZA MGANGA MFAWIDHI KITUO CHA AFYA BUHINGU KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU

Tarehe: 19 Oct, 2023


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma  Thobias Andengenye amemuelekeza  Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Buhingu kilichopo wilayani Uvinza,  Amos Matariji kufuatia kulalamikiwa na wananchi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kuendana na Kanuni na Maadili ya Utumishi wa Umma.

Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo hayo alipozungumza  kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mgambo wilayani humo  akiwa katika ziara ya kikazi ambapo wakazi wameonesha kutoridhishwa  na utendaji kazi wa mtumishi huyo ikiwemo
kutokuwa muwazi katika  matumizi ya fedha za Umma, kutoa kauli zisizo za kimaadili na kutozingatia taratibu za utoaji huduma bora na kwa wakati.

Kupitia hadhara hiyo, Andengenye  amewakumbusha watumishi wa Umma kuachana na tabia zisizo za kimaadili ikiwemo utovu wa nidhamu wanapotekeleza  majukumu ya kuwahudumia wananchi.

Pia amewasisitiza watendaji wa vijiji kuzingatia taratibu za vikao vya kisheria ikiwa ni pamoja na  kusoma taarifa za mapato na matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa katika maeneo yao kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Katika kuhakikisha jamii inawajibika, kiongozi huyo ametoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kushiriki mikutano ya vijiji  ili  kupokea taarifa za kiutendaji katika maeneo yao na kupata fursa ya kuchangia mawazo.

Upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba ameahidi kuchukua hatua za kinidhamu ikiwemo kumbadilishia kituo cha kazi  mtumishi huyo.

"Tumefuatilia na kubaini uwepo wa changamoto za kiutendaji kazi kwa mtumishi huyo hivyo ndani ya siku saba atabadilishiwa kituo cha kazi  na kutoendelea kuwa mganga mfawidhi huku akitekeleza majukumu yake chini ya uangalizi" amesisitiza Lebba.

Katika hatua nyingine Dkt. Lebba amewaasa wakazi kuendelea kushirikiana na wataalam wa Afya katika kupambana na maradhi ikiwemo changamoto za maradhi ya tumbo kwa kuimarisha hali ya usafi wa vyakula, Maji na Mazingira nyakati zote.
..........................
Tufuatilie zaidi kupitia
#instagram @mainfmtanzania
#facebook @mainfmtanzania
#twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab