National News

WANANCHI MKOANI KIGOMA WAPATA ELIMU YA KUKABILIANA NA MAJANGA

Tarehe: 18 Oct, 2023


Wananchi wa Wilaya ya Uvinza Leo Oktoba 18, 2023 wamepatiwa mafunzo namna ya kujikinga na kukabiliana na Majanga mbalimbali. 

Elimu hiyo imetolewa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu idara ya Menejimenti ya Maafa katika Ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza kwa Wajumbe wa Kamati za Kata za Uvinza, Kandaga na Kazuramimba.

Awali akifungua Mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Naibu Kamishina Hamisi Mrutengo amewataka Wajumbe wa  Kamati za Maafa ngazi za Kata kuzingatia elimu watakayoipata kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na majanga katika jamii zao.

Amesema jamii ni lazima iendelee kupewa mafunzo na mazoezi ya namna ya kukabiliana na     Majanga ya Asili na yanayosababishwa na Shughuli za Kibinadamu ili kupunguza madhara ya utegemezi, Umasikini na matumizi ya fedha nje ya Mipango.  

Naye Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dr. Mololo Noah  amewasilisha mada ya namna   Jamii inavyokabiliana na Maafa kupitia ngazi tofauti tofauti kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Taifa kulingana na ukubwa wa janga.

Aidha amewataka Wananchi kufanya mikutano na vikao vya mara kwa mara kuainisha majanga katika maeneo yao,  kufanya tathimini kabla ya Kutokea,  likitokea na baada ya tukio.

Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kigoma Ndugu. Msafiri Nzunuri amewataka wajumbe hao kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi pindi linapotokea janga kushirikiana katika hatua zote na kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika ķwa lengo la kurejesha hali kama vile ukarabati au ujenzi wa Miundombinu mbalimbali. 

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab