Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa-Kilolo (km 33.61) kwa kiwango cha lami utakapokamilika utaleta mageuzi chanya na kuchochea fursa nyingi katika Sekta ya Kilimo, Utali, Biashara na Uwekezaji.
Bashungwa ameongeza kuwa kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kutawezesha wananchi kiuchumi, na kuwaondolea adha ya muda mrefu ya usafiri.
Aidha Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifahamu adha ya wana Iringa na mikoa jirani katika eneo la Kitonga na amemuagiza kufika na timu ya Watalaam kutoka TANROADS na kufanya tathimini ya ujenzi wa barabara ya mbadala ya muda mfupi wakati Serikali ikiendelea kutafuta dawa ya kudumu katika eneo hilo lenye mlima mkali.
Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass) yenye urefu wa kilometa 7.3 ambapo sasa hivi ipo katika hatua za manunuzi.
Bashunga pia amezitaja barabara nyingine ambazo zitakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami katika mkoa huo ikiwemo barabara ya Iringa - Ipagala (km 71),
Aidha, Bashungwa ametoa agizo kwa TANROADS kuusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara hiyo ili ijengwe kwa viwango vilivyoanishwa kwenye mkataba ili tuweze kupata thamani ya fedha ambazo Serikali imewekeza na barabara hiyo idumu kwa muda uliokusudiwa.
Awali akitoa taarifa ya mradi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mha. Mohamed Besta amesema kuwa mradi huu utatekekelezwa kwa muda wa miezi 24.