National News

SEKTA YA UTALII KUSHIRIKIANA NA WADAU KUTOKA NCHI MBALIMBALI

Tarehe: 28 Sep, 2023


Tanzania imejipanga kuendelea kushirikiana na wadau kutoka nchi mbalimbali duniani katika kukuza na kuendeleza Sekta ya utalii nchini. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika hafla ya Ufunguzi ya Siku ya Utalii Duniani liyofanyika jijini Riyadh, Saudi Arabia.

"Nimekutana na wenzetu wa Sekta ya Utalii kutoka nchi mbalimbali kama Israel, Indonesia, Miamar, Honduras, Senegal, Sierra Leon pamoja na Mawaziri wengine 45 kutoka nchi hizo ambapo tunaamini huu ni mwanzo mzuri kuhakikisha kwamba tunaendelea kuitangaza nchi yetu ili tuweze kupiga hatua kubwa zaidi." - Angellah Kairuki.

Ameongeza kuwa kupitia Mawaziri wa Utalii wa nchi nyingine walioshiriki maadhimisho hayo Tanzania ina mpango wa kukiunganisha Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na vyuo vingine vya nchi nyingine vilivyopo nje ya nchi ili viweze kushirikiana katika utoaji wa mafunzo kuhakikisha mafunzo yanayotolewa ni muafaka kulingana na huduma za kitalii ambazo watalii wanazihitaji.

"Tumefurahi kuona hapa Saudi Arabia leo hii wamezindua chuo cha mafunzo ya ukarimu na utalii na sisi Tanzania tumeonyesha nia ya kushirikiana nao katika mafunzo, tutakuwa na mazungumzo na Waziri wa Utalii wa hapa Saudi Arabia kuona ni namna gani Watanzania wanaweza kunufaika." Amesema Kairuki.

...............
Tufuatilie zaidi
Instagram @mainfmtanzania
Facebook @mainfmtanzania 
Twitter @mainfmtanzania

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab