National News

WAZIRI MKUU KUUNDA TIMU KUCHUNGUZA UPIGAJI FEDHA KIGOMA

Tarehe: 22 Sep, 2023


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atapeleka timu maalum ya uchunguzi wilayani Kigoma ili ifanye uchunguzi wa fedha zinazopotea kinyemela kupitia mtandao wa watumishi wasio waaminifu.


Waziri mkuu ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Septemba 22, 2023) wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma mjini ambapo amesema fedha zinazotoka Serikali Kuu huwa zinatumwa na maelekezo mahsusi ya  kwamba zinaenda kufanya shughuli gani na  za makusanyo ya ndani maamuzi ya matumizi yake ni lazima yafanywe na Baraza lote la Madiwani. 


“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti   kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” amesema.

 

Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema Manispaa ya Kigoma ilipokea sh. milioni 500 kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI zikakaa kwenye akaunti kwa muda mrefu lakini baadaye zikatoweka na hazijulikani zilitumika kufanya nini.

 

“Kuna kiasi kingine cha shilingi milioni 447 kilitumwa Kigoma, wakati zinaandaliwa kutoka, Mkurugenzi akazuia. Hongera Mkurugenzi na uendelee kuzizuia, sisi tunamfuatilia Mkurugenzi aliyekuwepo kwa sababu anajua zile shilingi milioni 500 zilitokaje.”Amesema

 

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Waziri Mkuu amesema wao wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo matumizi mabaya ya fedha, makusanyo kidogo sababu ya malumbano, mawakala kukaa na fedha mikononi badala ya kuzipeleka benki, Baraza la Madiwani kukosa taarifa za fedha na kutumia fedha za miradi kulipana posho.

 

“Kuna watu wamejilipa shilingi milioni 11 zikiwa ni posho ya safari ya Dodoma. Pia wametumia shilingi milioni sita kufanya service ya gari, hili ni gari la aina gani? Wengine wametumia shilingi milioni 9 kwenye sherehe za Siku ya Mtoto wa Afrika na wengine wamejilipa shilingi milioni 14. 8 kwenda kwenye sherehe za Nane Nane Tabora, hivi mlikaa siku ngapi huko?”, alihoji Waziri Mkuu.

 

Aidha waziri Mkuu amesema kuna tume ya TAMISEMI ilikwenda kufanya uchunguzi kwenye Halmashauri hiyo kuhusiana na matatizo hayo ambapo  ameitaka tume hiyo ikamilishe kazi yake haraka na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi, OR TAMISEMI.


“Tume ikamilishe kazi haraka, akabidhiwe Waziri. Namwagiza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa akipokea taarifa ya tume hiyo, aje Kigoma achukue hatua,” amesema.

  • © Copyright - 2024
  • All rights reserved by - MainFm
  • Developed by - Mainfintech Lab