National News

MCHENGERWA AWATAKA WATANZANIA KUILINDA MIUNDOMINU ILIYOTEKELEZWA NA SERIKALI

Tarehe: 14 Sep, 2023


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amemtaka kila mtanzania kuwa mlinzi wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa nchini kwa kutoa taarifa za ubadhilifu wa fedha ili iwe na tija kwa jamii na maendeleo ya taifa  kwa watanzania ikiwa ni pamoja na  ile ya afya na elimu iliyojengwa na Serikali ili inufaishe kizazi cha sasa na kijacho.

Mchengerwa ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi  wa Kijiji cha Nyamwage Kata ya Mbwara wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Rufiji pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma walio katika Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Akizungumzia kiasi cha fedha kilichopokelewa katika Hamashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Abdul Chobo amesema halmashauri yake ilipokea shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa  shule kongwe na ujenzi unaendelea vizuri ili wanafunzi wawe na mazingira rafiki ya kupata elimu bora.

Sanjari na hilo, Mhe. Chobo amesema Halmashauri yake ilipokea zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu sita hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawezesha walimu kupata makazi bora.

Katika hatua nyingine ameongeza kuwa walipokea fedha za Mradi wa BOOST kiasi cha shilingi milioni 916 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ambazo zimetatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi darasani, wanafunzi kukaa chini na upungufu wa madarasa.