MADEREVA VYOMBO VYA MOTO WATAKIWA KUTII SHERIA BARABARANI
Tarehe: 13 Sep, 2023
Katika kuzuia ajali za barabarani jeshi la polisi Mkoani Kigoma limeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa vyombo vya moto, utoaji wa elimu kwa watumiaji wa barabara wakiwemo madereva na watembea kwa miguu.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma ACP Filemon Makungu amesema kuwa kwa kipindi cha tangu tarehe 1 Agosti, 2023 hadi tarehe 11 Septemba, 2023 jumla ya makosa 6,870 ya usalama barabarani yamekamatwa na kutozwa faini ambapo madereva (13) wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwa ni pamoja na mwendokasi, kuzidisha abiria na kupita magari mengine (wrong overtaking) katika maeneo hatarishi hususani kwenye kona, pia madereva wawili (2) wamefungiwa leseni zao za udereva baada ya kukiuka sheria hizo
Aidha Jeshi la Polisi limewasihi madereva mkoani Kigoma na nchi nzima kwa ujumla kuendelea kutii na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea kutokana na uzembe