National News

POLISI YAMSAKA MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANAUME SAME

Tarehe: 16 Oct, 2026


Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Peter Kiariro, mkazi wa Maore, Wilaya ya Same, kwa tuhuma za kumuua Bernard Kiluwa, mwenye umri wa miaka 26.


Tukio hilo limetokea usiku wa Oktoba 12, 2026, katika Kitongoji cha Kalemane, Kijiji cha Mheza, Tarafa ya Ndungu, wilayani Same.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi, kufuatia marehemu kucheza muziki kwa muda mrefu na mke wa mtuhumiwa katika sherehe ya ubarikio.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimwita marehemu pembeni kwa mazungumzo, lakini baadaye akamshambulia kwa kitu chenye ncha kali kifuani na tumboni kabla ya kutoroka eneo la tukio.

Bernard alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Ndungu.

Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa ili akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, huku likiwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.