Hali ya Usafiri na usafirishaji katika kata za Mwilamvya na Kimobwa zilizopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mkoani Kigoma imeendelea kuimarika kufuatia ujenzi wa barabara inayounganisha kata hizo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya Kata.
Wakizungumzia utekelezaji wa mradi huo wa barabara, Wananchi wa Kata ya Mwilamvya wamesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka shambani, sambamba na kutatua changamoto ya usafiri katika kata hizo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwilamvya, Emmanuel Gamuye amesema kuwa barabara hiyo itafungua mitaa kwa baadhi ya wananchi ambao makazi yao yalikuwa hayafikiki kwa urahisi, sambamba na kurahisisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, huku akiwataka wananchi ambao barabara imepita katika maeneo ya mashamba yao kuendelea kuwa watulivu kwani ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya maendeleo kwa wananchi.
Nae, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwilamvya, Idd Emmanuel Daud ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii baina ya kata hizo mbili, ambapo wananchi watakuwa na uwezo wa kuingia na kutoka katika kata hizo kwa urahisi zaidi kufuata huduma hizo.