JAMII YATAKIWA KUWAJALI WAFUNGWA KWA KUWAPATIA MISAADA
Tarehe: 08 Oct, 2026
Jamii imetakiwa kuendelea kuwajali wafungwa kwa kuwapatia misaada mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuwaonyesha upendo na kuwathamini licha ya makosa yaliyowafanya kuwa gerezani.
Wito huo umetolewa na Mrakibu Msaidizi wa Magereza katika Gereza la Bangwe mkoani Kigoma, Mary Mwendasila, wakati akizungumza baada ya kupokea msaada kutoka kwa watumishi wa Shirika la Posta mkoani Kigoma waliotembelea gereza hilo kwa ajili ya kutoa msaada.
Mary amesema katika dhana ya urekebishaji wa wafungwa, hatua hiyo hufanikiwa zaidi pale wafungwa wanapoamini kuwa jamii iliyopo nje ya gereza bado inawapenda, kuwathamini na kuwajali.
Ameitaka jamii kuendelea kuwapelekea wafungwa misaada ya vitu mbalimbali, ikiwemo vifaa vya usafi, taulo za kike na mahitaji mengine muhimu.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Kigoma, Bw. Ndagije Chobariko, amesema wameamua kutoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kile kidogo wanachokipata.
Amesema pia msaada huo ni sehemu ya kuendelea kuihamasisha jamii kuwajali wafungwa kwa kuwatembelea na kuwapelekea mahitaji mbalimbali wanayohitaji.