National News

HIMIZENI WANANCHI KUSHIRIKI UJENZI WA VYOO SHULENI - CPA KAFUKU

Tarehe: 06 Oct, 2026


Watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, wameagizwa kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vyoo mashuleni, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Halmashauri hiyo kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyoo katika shule za msingi na sekondari.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, CPA Francis Kafuku, wakati wa kikao maalumu kilichowakutanisha Watendaji wa Kata na Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji pamoja na baadhi ya Walimu Wakuu, kwa lengo la kujadili namna ya kuwashirikisha wananchi katika kutatua changamoto ya vyoo mashuleni.

CPA Kafuku amesema viongozi hao wana nafasi kubwa katika kufanikisha zoezi hilo kutokana na kuwa karibu na wananchi, hivyo wanapaswa kutumia nafasi zao kuwahamasisha wananchi kushiriki katika ujenzi wa vyoo ili kuondokana na changamoto hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Halmashauri hiyo, Rebeka Ezra, amesema Halmashauri tayari imetenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vyoo 253 katika shule mbalimbali, ambapo ameeleza kuwa kati ya vyoo hivyo, vyoo 215 vitajengwa katika shule za msingi, huku vyoo 38 vikijengwa katika shule za sekondari.

Nao baadhi ya viongozi walioshiriki kikao hicho wameeleza kuwa wako tayari kushirikiana na wananchi katika utekelezaji wa zoezi hilo, wakisisitiza kuwa changamoto ya vyoo mashuleni ni jukumu la jamii nzima na linahitaji ushirikiano wa pamoja.