DC MATHAMANI AWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA EL NINÕ
Tarehe: 27 Sep, 2026
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinah Mathamani, amewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema dhidi ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi kijacho, kwa kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ruchugi, Kata ya Uvinza, Mheshimiwa Dinah amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiwekea mahitaji muhimu ya msingi majumbani, pamoja na kushirikiana katika kuboresha miundombinu na kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka.
Amesema hatua hizo zitasaidia kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi katika mifereji na maeneo ya kupitisha maji, hivyo kupunguza uwezekano wa mafuriko na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
“Tuchukue tahadhari mapema, tuweke mazingira yetu katika hali salama na tuwe tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua,” amesema Mheshimiwa Dinah.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kuzingatia maelekezo ya tahadhari na kuchukua hatua za kujilinda wao wenyewe, familia zao na mali zao ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo.