DC CHUACHUA AKABIDHI MAGUTA 6 KUIMARISHA USAFI KIGOMA UJIJI
Tarehe: 19 Sep, 2026
Manispaa ya Kigoma Ujiji imekabidhi pikipiki sita za magurudumu matatu maarufu kama maguta, kwa ajili ya kusaidia zoezi la usafi wa mazingira, hususani uzoaji wa taka zinazokusanywa na kurundikwa katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa maguta hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, amesema maguta hayo yatasaidia kuzoa taka kutoka katika maeneo ambayo zimekuwa zikikusanywa, lakini amesisitiza kuwa vifaa hivyo pekee haviwezi kubadilisha tabia za wananchi wanaochafua mazingira.
Amesema ni muhimu wananchi wanaochafua mazingira kwa makusudi kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kulipishwa faini, ili kuongeza uwajibikaji katika suala la usafi wa mazingira.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Petronila Gwakila, amesema maguta hayo yamekabidhiwa kwa kata sita za Manispaa hiyo zenye uzalishaji mkubwa wa taka, kwa ajili ya kusaidia shughuli za usafi.
Amesema pikipiki hizo zimenunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Manispaa na zimegharimu jumla ya Shilingi milioni 53 na Laki 1.