National News

RC SIRRO ATOA MAELEKEZO KWA TANROADS NA TARURA KIGOMA KUKABILIANA NA EL NINO

Tarehe: 06 Sep, 2026


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amezielekeza mamlaka za TARURA na TANROADS kuhakikisha mitaro yote katika mkoa huo inasafishwa na kuwekwa katika hali nzuri ili iweze kupitisha maji ya mvua, wakati mkoa huo ukijiandaa kukabiliana na mvua za El NiƱo zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Balozi Sirro amesema Mkoa wa Kigoma umekuwa ukikabiliwa na athari za mvua za vuli kutokana na kuwepo kwa makorongo mengi, hali inayoweza kuongeza madhara endapo maandalizi ya mapema hayatafanyika.

Amesema TARURA na TANROADS zinapaswa kuhakikisha mitaro yote inasafishwa na kuwekwa katika hali inayokidhi mahitaji ya kupitisha maji kwa ufanisi, hatua ambayo itasaidia kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi kwa kusafisha mifereji na kuondoa taka zinazoweza kuziba njia za maji.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya mamlaka husika na wananchi ni muhimu katika kujiandaa mapema na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.