National News

UZEMBE WATAJWA KUCHELEWA SOKO LA MWANGA MANISPAA YA KIGOMA UJIJI

Tarehe: 24 Aug, 2026


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho, leo amefanya ziara katika Soko la Mwanga jijini Kigoma, akikagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo la kisasa.


Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali walishiriki, akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, ambaye ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Baba Levo amesema kuna uzembe katika utekelezaji wa ujenzi huo na kuwataka wahusika kuwajibika, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili ili wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla waweze kunufaika.

Aidha, ziara hiyo ilihudhuriwa na Mhe. Zainabu Athumani Katimba, ambaye amesisitiza umuhimu wa Soko la Mwanga katika kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani Kigoma.

Viongozi hao wamewataka wasimamizi wa mradi kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo, ili wananchi wapate thamani halisi ya mradi huo unaotarajiwa kuongeza tija na mapato ya Manispaa ya Kigoma.