Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi, wameingia makubaliano ya kimkakati ya kushirikiana katika sekta ya madini kupitia ubadilishanaji wa ujuzi, uchimbaji, uongezaji thamani na utafutaji wa masoko.
Makubaliano hayo yamefanyika Ikulu Ndogo visiwani Zanzibar, ambapo Rais Samia pia ameialika rasmi DRC kujiunga na Kituo cha Madini cha Afrika Mashariki na Kati kwa ajili ya kuimarisha tafiti za pamoja.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya siku mbili nchini, Rais Tshisekedi amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuungana kulinda na kunufaika na rasilimali zao, akibainisha kuwa bara hilo limechoshwa na wizi wa madini unaoendelea.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kubadilisha muelekeo wa sekta hiyo ili kuhakikisha faida ya moja kwa moja inabaki kwa wananchi wa Afrika. Rais Tshisekedi ameongeza kuwa ili kufikia azma hiyo, ni lazima nchi za Afrika ziwekeze kwenye miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, bandari na nishati ya umeme ya kiwango cha juu.
Amesisitiza kuwa mshikamano huo unaleta taswira mpya inayofuatiliwa kwa ukaribu na mataifa ya nje, ikiwemo ya Bara la Ulaya, na wapo tayari kusimama imara kuhakikisha maono hayo ya kiuchumi yanatimia kikamilifu.