National News

ZIMAMOTO KASULU YAWATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA ZA MOTO KWA WAKATI

Tarehe: 17 Aug, 2026


Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, limewataka wananchi kutoa taarifa kwa wakati pindi majanga ya moto yanapotokea, ili kuliwezesha jeshi hilo kufika kwa haraka katika maeneo ya matukio na kudhibiti madhara, badala ya kulalamikia ucheleweshaji wa huduma ilihali taarifa imetolewa kwa kuchelewa.


Wito huo umetolewa na Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu, Mrakibu Msaidizi Anthony Marwa, wakati akitoa elimu kwa walimu wa Shule ya Sekondari Bogwe kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Marwa amesema wananchi wengi wamekuwa na tabia ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji baada ya moto kuwa mkubwa, hali inayochangia kuongezeka kwa madhara, ambapo amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa mapema utaliwezesha jeshi hilo kuchukua hatua kwa haraka na kupunguza muda wa kutoka kituoni hadi kufika eneo la tukio.

Aidha, Marwa amewataka wananchi kuacha utaratibu wa kuwasiliana na Jeshi la Polisi wanapotaka kuripoti majanga ya moto, na badala yake kuwasiliana moja kwa moja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia namba 114, hatua ambayo itasaidia kupunguza ucheleweshaji wa taarifa na kuongeza ufanisi wa huduma za uokoaji.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu limeendelea kutoa elimu kwa walimu, walimu wakuu na wamiliki wa shule mbalimbali zenye mabweni, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto, pamoja na kuhakikisha wanafunzi na jamii ya shule kwa ujumla wanakuwa na uelewa wa hatua za kuchukua wakati wa dharura.

Elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu namna ya kuzuia majanga ya moto, kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kwa wakati ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pale majanga hayo yanapotokea.