WAANDISHI WA HABARI KIGOMA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU UGONJWA WA SIKOSELI
Tarehe: 08 Sep, 2023
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni- Kigoma imetoa mafunzo ya ugonjwa wa sikoseli kwa waandishi wa habari Mkoa wa Kigoma kutoka katika vyombo vya habari 20 kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili waweze kupata uelewa na kuweza kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma. Ikiwa ni kuadhimisha mwezi wa uelimishaji juu ya ugojwa wa sikoseli Duniani, ambayo hufanyika mwezi Septemba kila mwaka.
Katika mafunzo hayo, Dkt, Macrice Yakayashi, Daktari bingwa wa Watoto na Mkuu wa Idara ya Watoto amesema, ili kupunguza wagojwa wa sikoseli katika Mkoa wa Kigoma wananchi wanatakiwa kuchukua hatua ya kufanya vipimo ili kubaini ugonjwa huo mapema
Aidha Dkt, Macrice Yakayashi amewataka wanandoa na wanaotarajia kufunga ndoa kujitokeza kufanya vipimo katika vituo vya Afya ili kupunguza uwezekano wa kupata wagonjwa wengi zaidi katika kipindi cha mbeleni.
Nae Dkt. Esther Peter Okelo kutoka idara ya Watoto, ambaye ametoa mafunzo hayo amewaomba wanahabari wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha wanayachukua waliyo jifunza na kwenda kuyasema kupitia radio na Televisheni ili wananchi waweze kupata elimu hiyo.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Press Club Mkoa wa Kigoma, ameishukuru Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni kwa kuandaa mafunzo ya ugonjwa wa sikoseli kwa ajili ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari Mkoani Kigoma na pia ameiomba hospitali kuendelea kutoa elimu ya magonjwa mbalimbali kwa waandishi wa habari ili waendelee kutoa elimu hiyo kwa jamii.