JESHI LA ZIMAMOTO KASULU LAWATAKA WANANCHI KUWASILISHA RAMANI ZA NYUMBA ZAO KABLA YA UJENZI
Tarehe: 14 Aug, 2026
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma limewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuwasilisha ramani za majengo katika ofisi za Jeshi hilo kabla ya kuanza ujenzi, ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kujenga kwa kuzingatia usalama na kinga dhidi ya majanga ya moto.
Wito huo umetolewa siku ya tarehe 14 agosti 2026 na Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu, Mrakibu Msaidizi Anthony Marwa, wakati wa zoezi la kutoa elimu kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa walimu wa Shule ya Sekondari Bogwe.
Marwa amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati inayotekelezwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kuzuia na kupunguza majanga ya moto, hususan katika shule na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu, ambapo amesema kuwa wananchi wanapaswa kufika katika ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya kupata elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali ya usalama dhidi ya moto, badala ya kusubiri majanga yatokee.
Kwa upande wake, askari wa Jeshi hilo, CF Christopher Sali Moses, wakati akitoa mafunzo kwa walimu hao, ameeleza umuhimu wa kutumia njia sahihi za kuzima moto kulingana na chanzo chake, ambapo amesema endapo moto umetokana na hitilafu ya umeme, hatua ya kwanza ni kuzima chanzo cha umeme, kisha kutumia kifaa kinachofaa kuzima moto huo, ikiwemo kizimamoto chenye gesi ya kabonidayoksaidi ili kuzuia madhara zaidi.
Nao baadhi ya walimu walioshiriki mafunzo hayo wamesema wamepata elimu muhimu itakayowawezesha kuchukua hatua za awali za usalama wakati wa kutokea kwa moto, huku wakisubiri msaada wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, huku wakiahidi kuifikisha elimu waliyoipata kwa wananchi wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha kinga dhidi ya majanga ya moto katika jamii.