#KIGOMA: Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania Bw.Ferdinand Kabyemela ametoa rai kwa wafanyabiashara mkoani Kigoma na taifa kwa ujumla, kutumia huduma (EMS) inayotolewa na shirika hilo kusafirisha mizigo kwenda kwenye mataifa zaidi ya 192 ambao ni wanachama wa Posta duniani, pamoja na mataifa mengine ambayo siyo wanachama.
Bw.Kabyemela ametoa rai hiyo leo 12 Agosti, 2026 wakati akizungumza Waandishi wa habari mkoani Kigoma kuhusu namna ambavyo shirika hilo limeboresha huduma zake kwa sasa, na kwamba huduma unayoipata kupitia (EMS) ni huduma ya viwango vya kimataifa pamoja ambapo pia mfanyabiashara ataweza kulifikia soko la kimataifa kwa urahisi zaidi na kwa uhakika.
Akielezea kuhusiana na utofauti wa Posta na taasisi nyingine Mkurugenzi wa Huduma za Posta wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Arubee Ngaruka, amesema kuwa ukisafirisha mzigo, nyaraka, bidhaa, vifurushi na nyinginezo kwa kutumia shirika hilo unakuwa na uwezo wa kufuatilia na kujua maendeleo ya mzigo wako hadi unafika sehemu husika kwa muda wote wa usafirishaji.
Vilevile Bw.Ngaruka amesema kuwa shirika hilo linasafirisha mizigo na vitu vyote ambavyo vimeruhusiwa kisheria na ni halali, huku akiwasihi wafanyabiashara na watu wengine kutumia shirika la Posta kusafirisha vitu kutokana na maboresho ambayo yamefanyika katika utoaji wa huduma hiyo uhakika zaidi na huduma ni ya viwango vya kimataifa.