National News

POLISI YASHIRIKI MATUKIO YA KIJAMII KUIMARISHA UHUSIANO NA JAMII

Tarehe: 10 Aug, 2026


Jeshi la Polisi kupitia Polisi Kata limeendelea kujenga na kuimarisha uhusiano pamoja na ushirikiano mzuri na jamii, kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kuwa karibu na wananchi, hatua inayolenga kuongeza uaminifu, usalama na utulivu katika maeneo yao.


Hayo yamebainika katika Kata ya Nyamnyusi, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma, ambapo Polisi Kata wa eneo hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa, amekutana na baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Kagembe B na kufanya nao mazungumzo ya kawaida.

Katika mazungumzo hayo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiusalama, akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuwaogopa polisi bali kuwaona kama wadau muhimu katika kulinda amani na usalama wa jamii.

Amesema ushirikiano wa karibu kati ya polisi na wananchi ni muhimu katika kubaini na kukabiliana na changamoto za kiusalama, pamoja na kujenga mazingira salama kwa jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Kagembe B wamesema mahusiano kati yao na Jeshi la Polisi yameendelea kuwa mazuri kutokana na uwepo na ushiriki wa Polisi Kata katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Wananchi hao wamesema wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, hali ambayo imeongeza uaminifu na kuwafanya wajisikie salama zaidi wanapokuwa na polisi katika shughuli zao za kila siku.