KAKONKO YAANZISHA BENKI YA TOFALI KUHARAKISHA UJENZI WA VYOO SHULENI
Tarehe: 06 Aug, 2026
Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma imeanzisha mkakati wa kuunda Benki ya Tofali ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuharakisha uboreshaji wa miundombinu ya elimu, hususan ujenzi wa vyoo vya wanafunzi katika shule za halmashauri hiyo, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kilichojadili taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata mbalimbali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli, amewataka watendaji wa kata kuhakikisha zoezi la ufyatuaji wa matofali linasimamiwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, ili kuondoa ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyoo pindi itakapoanza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Fidel Nderego, amesema wilaya hiyo inaendelea kushuhudia ongezeko la kasi ya maendeleo ikilinganishwa na miaka iliyopita, ambapo amewahimiza madiwani na watendaji kuongeza bidii, ushirikiano na uwajibikaji ili kuhakikisha mafanikio hayo yanaimarishwa na kuwanufaisha wananchi zaidi.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa, amesisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya elimu yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, ambapo amewataka watumishi wa umma, viongozi na wananchi kushiriki kikamilifu katika kuboresha elimu kwa kuwalea na kuwaongoza watoto, badala ya kuliachia jukumu hilo walimu pekee.