Nahodha wa SC villa ya Uganda Afariki Kwa Kushwambuliwa Na Watu Wanaodaiwa Kuwa Majambazi
Tarehe: 05 Aug, 2026
Nahodha wa klabu ya SC Villa ya Uganda, David Owori amefariki dunia baada ya kushambuliwa na Watu wanaodaiwa kuwa majambazi alipokuwa akirejea nyumbani usiku wa Agosti 4, 2026.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Klabu hiyo, ikieleza kuwa aliachwa akiwa katika hali mahututi kufuatia shambulio hilo kabla ya kufariki dunia. Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo lilitokea karibu na Makazi yake, ambapo washambuliaji wanaoaminika kuwa majambazi walimvamia na kumjeruhi vibaya.
Inaelezwa kuwa licha ya juhudi za kuokoa maisha yake, Owori alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata. Kifo chake kinakuja siku chache baada ya kuiongoza SC Villa katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la FUFA, jambo ambalo limeacha mshtuko mkubwa kwa Mashabiki, Wachezaji wenzake na familia ya soka Nchini Uganda.
SC Villa imetoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, marafiki na wadau wa soka, ikimtaja Owori kama kiongozi aliyejitolea na mwenye mchango mkubwa ndani na nje ya uwanja, Polisi Nchini Uganda wamesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.