WHO YAOMBA MSAADA ZAIDI ILI KUKABILIANA NA MLIPUKO WA EBOLA
Tarehe: 05 Aug, 2026
Shirika la Afya Duniani - WHO limetoa wito wa msaada zaidi kwa pande zote ili kupambana na mlipuko wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambao bado unazidi kuwa changamoto kubwa.
Mlipuko huo ni mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Kongo, licha ya kutangazwa chini ya miezi mitatu iliyopita. Msemaji wa WHO Tarik Jasarevic aliwaambia waandishi wa habari huko Geneva kuwa kwa bahati mbaya mlipuko huo wa Ebolabado unaongezeka zaidi licha ya juhudi zinazoendelea.
Amesema wanahitaji msaada zaidi katika upande wa fedha, lakini pia rasilimali zingine ili kuimarisha juhudi zote za kukabiliana na janga hilo ikiwemo uwezo wa matibabu, timu za uchunguzi, timu za kuendesha mazishi kwa njia salama na wafanyakazi wa jamii.
Kumekuwa na visa 3,802 vilivyothibitishwa vya Ebola nchini Kongo, ikiwa ni pamoja na vifo 1,707. Jumla ya wagonjwa 727 wamepona, na kuna visa 275 vinavyoshukiwa kuwa vya kirusi hicho ambavyo vinachunguzwa.