National News

POKEENI WAGENI KWA KUZINGATIA SHERIA ZA UHAMIAJI - AFANDE LUPA

Tarehe: 04 Aug, 2026


Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, iliyopo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa, amewataka wananchi wa kata hiyo, hususan wakazi wa Kitongoji cha Muhanga, kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za uhamiaji wanapowapokea wageni kutoka nchi jirani, ili kudhibiti na kutokomeza tatizo la uhamiaji haramu.


Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Muhanga, Kijiji cha Mkieta, Lupa amesema kuwa ataendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi katika mapambano dhidi ya uhamiaji haramu, ambapo ameeleza kuwa atatoa taarifa kwa mamlaka husika pale atakapobaini uwepo wa wahamiaji haramu, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkieta, Hassan Kisema Ninkuli, amewasisitiza wananchi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Polisi Kata, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuimarisha usalama wa kijiji na kuzuia changamoto zinazoweza kusababishwa na uwepo wa wahamiaji haramu.

Nao baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Muhanga wameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya uhamiaji haramu, huku wakimpongeza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Willy Lupa kwa ushirikiano wake wa karibu na wananchi pamoja na juhudi zake za kuimarisha usalama katika eneo hilo.