UTORO WAZUA WASIWASI SHULE YA MSINGI MUHANGA KASULU
Tarehe: 04 Aug, 2026
Wananchi wa Kitongoji cha Muhanga, kilichopo Kijiji cha Mkieta, Kata ya Nyamnyusi, Wilaya ya Kasulu, wameeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la utoro wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Muhanga, wakisema hali hiyo inatishia mustakabali wa elimu na maendeleo ya watoto, ambapo wametoa wito kwa Serikali pamoja na wadau wa elimu kuchukua hatua za haraka kukomesha tatizo hilo.
Wakizungumza kuhusu changamoto hiyo, wananchi hao wamesema utoro umeendelea kuongezeka licha ya jitihada zinazofanywa na walimu, ikiwemo kutoa adhabu kwa wanafunzi wanaokiuka taratibu za shule, huku wakieleza kuwa baadhi ya wazazi wanakabiliwa na ugumu wa kusimamia malezi ya watoto kutokana na tabia zisizofaa zinazochangia kutohudhuria masomo.
Hata hivyo, wameahidi kuendelea kushirikiana na walimu katika kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkieta, Hassan Kisema Ninkuli, amesema Serikali ya Kijiji imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo hilo, ikiwemo kuitisha kikao cha Kamati ya Shule ili kubaini chanzo cha utoro pamoja na kutoa elimu kwa wazazi kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha watoto wanarejea shuleni.
Nae, Mwalimu Richard Thomaso, aliyezungumza kwa niaba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muhanga, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuwahimiza watoto kuhudhuria masomo ili wapate haki yao ya msingi ya elimu.
Akizungumzia suala hilo, Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi William Lupa, amekemea vitendo vya utoro akisema kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia watoto kujiingiza katika makundi ya uhalifu, ambapo amesema kupitia mradi wa kuwarejesha wanafunzi shuleni, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine litahakikisha tatizo la utoro linadhibitiwa na kutokomezwa katika Shule ya Msingi Muhanga.