RAIS MUSEVEN AWATAKA WAZAZI KUTATHMINI UPYA MAHARI WANAZOTOZA KWA VIJANA WAOAJI
Tarehe: 03 Aug, 2026
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amewataka wazazi kupunguza kiwango cha Mahari wanachodai wakati wa kuwaozesha mabinti zao, akisema kuwa desturi ya kudai mahari kubwa imekuwa ikiwazuia vijana wengi kuingia kwenye ndoa.
Akizungumza katika harusi ya afisa mmoja wa serikali iliyofanyika Wilayani Kiruhura, Magharibi mwa Uganda, Museveni alisema baadhi ya familia zimegeuza mahari kuwa njia ya kujipatia utajiri, jambo ambalo, kwa maoni yake, linachangia kupungua kwa idadi ya ndoa nchini.
Alisisitiza kuwa mahitaji makubwa ya fedha na mifugo kama mahari yanawaongezea vijana mzigo mkubwa wa kifedha, hali inayowafanya wengi kuahirisha au hata kuachana kabisa na mipango ya kuoa.
Kauli za Museveni zimezua mjadala mpya kuhusu iwapo desturi za mahari zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa vijana, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda mila na tamaduni za jamii.