POLISI WAHIMIZA USHIRIKIANO KATIKA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA NYAMNYUSI
Tarehe: 03 Aug, 2026
Wananchi wa Kitongoji cha Muhenga, kilichopo Kijiji cha Mkieta, Kata ya Nyamnyusi, Wilayani Kasulu, wametakiwa kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo lao kwa kutoa taarifa sahihii kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha amani ya jamii.
Wito huo umetolewa na Polisi Kata wa Kata ya Nyamnyusi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, William Lupa, wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika Kitongoji cha Muhenga na kushirikisha viongozi wa kata, kijiji pamoja na wananchi, ambapo amesema kuwa usalama wa jamii ni jukumu la kila mwananchi, hivyo ni muhimu kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu mapema ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na matukio ya kihalifu yazuiwe kabla hayajatokea.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Muhenga amesema zoezi la usafi wa mazingira litafanyika mara kwa mara ili kuhakikisha mazingira ya kitongoji hicho yanabaki safi na salama, huku akiiomba Serikali kuboresha miundombinu ya soko la kitongoji hicho, akieleza kuwa wafanyabiashara hukumbana na changamoto kubwa wakati wa msimu wa mvua kutokana na mazingira yasiyoridhisha.
Nao baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Muhenga wamepongeza uongozi wa Kata ya Nyamnyusi pamoja na Polisi Kata kwa kuandaa zoezi hilo la usafi wa mazingira, wakisema limeongeza mshikamano miongoni mwa wananchi na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Vilevile, wameeleza kuwa hilo ni zoezi la kwanza la aina hiyo kufanyika katika kitongoji hicho na wameomba liwe endelevu kwa manufaa ya jamii.