National News

WAKULIMA WILAYA YA KASULU WAGAWIWA MICHE MIL. 1.3 YA KAHAWA

Tarehe: 18 Nov, 2025


#KIGOMA:Zaidi ya miche Milioni 1.3 ya Kahawa imegawiwa kwa wakulima zaidi ya 1000 katika Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma kwa lengo la kukuza na kuendeleza kilimo cha zao la Kahawa katika halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mratibu wa zao la Kahawa Halmashauri ya Mji Kasulu Bw. Eliakimu Charles amesema idadi ya maombi ya miche kutoka kwa wakulima ilikuwa kubwa kuliko miche iliyoandaliwa, nakueleza kuwa kwasasa mwitikio umekuwa mkubwa kuongezeka kwa wakulima wa zao la kahawa kutokana na Elimu wanayopatiwa.

Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye amesema ugawaji wa miche hiyo ni zoezi endelevu kwakuwa Serikali imeweka mkazo katika kumwezesha mkulima na kuhakikisha ananufaika kilimo cha zao la kahawa.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amewataka wakulima kuhakikisha wanapanda miche hiyo ndani ya halmashauri hiyo na kuitunza ipasavyo ili iweze kuwanufaisha na kubainisha kuwa serikali iko tayari kuwatafutia masoko wakulima hao ili kuhakikisha zao la kahawa linaongezeka thamani huku baadhi ya wakulima wa zao hilo katika hiyo wakisema kahawa imeendelea kuwa na manufaa makubwa katika kukuza uchumi wao.