National News

SIRRO ATAKA UWAJIBIKAJI IDARA YA BIASHARA, KILIMO

Tarehe: 15 Jul, 2025


#KIGOMA:Mkuu wa mkoa wa Kigoma Simon Sirro amewataka viongozi wa idara za kilimo na biashara mkoani Kigoma kuwajibika katika usimamizi na utendaji wa kazi zao kwani ndio msingi wa maendeleo kwenye jamii.

Akizungumza katika kikao na watumishi wa serikali Manispaa ya Kigoma Ujiji kamanda Sirro ameongeza kuwa Maendeleo hayawezi kuja hivihivi bila watu kufanya kazi na kujituma ili kuleta mabadiliko katika jamii kwa kufanya kilimo biashara na ufugaji biashara ili kuepukana na dhana ya kufuga ama kulima kwaajili ya matumizi ya chakula pekee.

Kwa upande wake Afisa kilimo wa manispaa ya kigoma ujiji Octavian Adam Moshiro  amesema kuwa hadi Sasa wameweza kupiga hatua kubwa kwa kuwaelimisha wananchi juu ya kilimo bora na chakisasa pia kufuga kuku wa nyama na mayai pamoja na  ng'ombe wa maziwa.

Naye Afisa uwekezaji na biashara Mohamed Habibu Kiguga ameongeza kuwa hadi Sasa wananchi wameweza kutengeneza vikundi na kuanzisha biashara pia kuzitangaza katika maonesho ya nanenane na Sabasaba ili kuweza kutangaza biashara zao ikiwa ni pamoja na kukuza na kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi.