National News

RAIS SAMIA AWAKUMBUKA WAZEE WENYE UHITAJI KIGOMA

Tarehe: 17 Jan, 2025


#KIGOMA:Mkuu wa wilaya ya Kigoma Mkoani Kigoma Dkt.Rashidi Chuachua amewaomba wadau mbalimbali wenye taasisi zinazotoa misaada ya kibinadamu mkoani hapa kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kwa lengo la kumuunga mkono rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Chuachua ametoa kauli hiyo wakati akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye kwenye hafla ya utoaji wa mahitaji mbalimbali kwa wazee wenye uhitaji katika kituo cha kulea Wazee cha Silabu kilichopo Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoni Kigoma iliyofanyika tarehe 16 Januari,2025 ikiwa ni zawadi kutoka kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kituo hicho.

"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa upendo na hekima kubwa, anayoionyesha kwa kuwagusa watu wenye uhitaji. Hakika pia niendelee kuwaomba Wanakigoma, wale ambao wanamiliki taasisi mbalimbali zinazotoa mahitaji ya kibinadamu waendeleaje kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa juhudi anazozifanya kwa kuhakikisha kuwa wanaendelea kuyagusa mahitaji watu wenye mahitaji maalumu".Alieleza Dkt.Chuachu
 
Nao baadhi ya Wazee wanaoishi katika kituo hicho wameishukuru serikali kwa zawadi hizo huku wakiiomba na wadau mbalimbali kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni Pamoja na kujengewa uzio ili kuondokana na changamoto ya wizi wa vitu mbalimbali katika eneo hilo.

"Tulikuwa tunaomba wadau wengine waendelee kutusaidia hapa tulipo. (Mzee mwingine aliongeza), sisi changamoto ya hapa kwetu ni wizi,uzio hamna tunaibiwa sana vitu hata huko bondeni mahindi yameisha mama utusaidie sana mama yangu kama unaweza kutusaidia kama ulivyotusaidia kwenye kula, tunakula tunanenepa".Walieleza baadhi ya Wazee.

Akijibu kuhusiana na baadhi ya changamoto mkuu wa wilaya ya Kigoma amesema kuwa serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum imepokea na itafanyia kazi ambapo zawadi mbalimbali zimetolewa ikiwa ni Pamoja na Sukari, Mchele na mbuzi wawili kwaajili ya kitoweo.