National News

JAPAN YAJA TANZANIA KUVUTIA WAWEKEZAJI

Tarehe: 15 Jan, 2025


#HABARI: Kampuni mbalimbali kutoka Japan zimewasili Tanzania kutathmini fursa za uwekezaji katika sekta za kilimo, utalii, na viwanda, ikiwa ni juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Katika kongamano la uwekezaji lililofanyika Januari 14, 2025, kampuni hizo zimekutana na kampuni 50 za Kitanzania kubadilishana uzoefu na teknolojia na pia kujadili miradi ya ushirikiano wa kibiashara.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa uwekezaji nchini, akibainisha kuwa Tanzania na Japan zina uhusiano wa muda mrefu katika sekta za maendeleo.

“Tunaendelea kushirikiana na Japan hasa katika miradi ya viwanda, barabara, na biashara. Hatua hii italeta ajira, teknolojia ya kisasa, na kuimarisha biashara ya nje,” alisema Kigahe.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Hisayuki Fujii, amepongeza uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, akisema mkutano huu umefungua milango ya uwekezaji mpya.

Mwekezaji Yoshiyuki Mizouchi wa kampuni ya Tanja inayojihusisha na kilimo Karatu, alisema: “Tumetoa ajira kwa Watanzania tangu 2023, na tunalenga kuvutia kampuni nyingine za Japan kuwekeza hapa.”

Hans Kejo wa kampuni ya Hamidu City Park ameongeza kuwa wana mipango ya kushirikiana na wawekezaji wa Japan, hususani katika teknolojia.

Kongamano hili linaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Japan.