KITILA ATAJA MAMBO SITA YALIYOCHOCHEA UCHUMI KUKUA
Tarehe: 11 Jan, 2025
#HABARI: Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa kitila Mkumbo ametaja mambo sita yaliyochochea uwekezaji mwaka 2024 kufikia usajili wa miradi 901.
Profesa Kitila amesema hayo leo Januari 10, 2025 katika kikao cha wizara hiyo alipozungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa 2025.
Amesema jambo la kwanza ni kuendelea kuimarisha mifumo ya kisera na sheria katika kuwezesha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na pili ni hamasa na ushawishi ambao umeendelea kufanywa na kuja kuwekeza nchini.
"Jambo la tatu ni kampeni kubwa ya kitaifa ya kuhamasishaji uwekezaji nchini iliyofanyika mwaka jana kwa ushirikiano mkubwa katika ya TIC, chemba za biashara nchini (TCCIA, TWCC), mabenki, na vyombo kampeni hii, katika mikoa 26 ya Tanzania bara; na wafanyabiashara 1800 walifikiwa,"amesema.
Pia, Profesa Kitila ametaja jambo lingine ni kuendelea kuimarishwa na kuboreshwa huduma kwa wawekezaji ndani ya TIC na nyingine ni kuanzishwa kwa ofisi mpya ya kanda ya kaskazini mkoani Arusha.
"Jambo la mwisho viongozi katika sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa, hususan wakuu wa mikoa, wameendelea kuhamasisha shughuli za uchumi na uwekezaji katika maeneo yao," amesema.