#HABARI: Mkuu wa wilaya ya Kigoma Dkt. Rashid Chuachua amesema Sekta ya usafirishaji ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kuinua na kukuza uchumi nchini na hivyo Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Bodaboda katika hilo.
Hayo ameyaeleza Januari 10, 2025 alipofanya mkutano na madereva bodaboda katika uwanja wa Kawawa kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa.
Akizungumza katika mkutano huo Dkt. Chuachua ametoa zuio kwa baadhi ya maafisa wa jeshi la polisi kutumia nguvu kubwa katika kuwasimamia madereva bodaboda ikiwa ni pamoja na kuwachapa fimbo na amewataka maderava hao kuendelea na shughuli zao za kila siku kwani usafiri huo ni nguzo muhimu katika jamii.
Katika hatua nyingine Dkt. Chuachua amewataka madereva ambao hawana leseni za udereva kusoma mafunzo maalumu kupitia vyuo vya ufundi Veta na kuhakikisha wanafuata Sheria za barabarani wawapo katika majukumu yao ya kila siku.
Nao baadhi ya madereva waliohudhuria mkutano huo wamesema uamuzi wa kukutana na mkuu wa Wilaya ni mzuri kwani mambo mbalimbali yamepatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kutatuliwa kwa baadhi ya kero zilizowasilishwa.
Ikumbukwe kuwa tarehe 9/01/2025 bodaboda walifanya maandamano wakishinikiza kile walichokiita kamatakamata inayofanywa na baadhi ya askari wa usalama barabarani huku wengine wakidai kupigwa na kutozwa faini kinyume na sheria.