KUWASA YASAINI MKATABA UJENZI TENKI LA MAJI LITA LAKI 2 KIGOMA
Tarehe: 13 Dec, 2024
#KIGOMA:Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) imesaini Mkataba na mkandarasi Datti Construction kwaajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa Tenki la Maji lenye ujazo wa lita laki mbili pamoja na ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilometa 9.4 kwaajili ya kumaliza changamoto ya Maji kwa wakazi wa maeneo ya Masanga na Mwasenga Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo ambao unagharimu shilingi milioni 836 fedha ambayo imetolewa na serikali, Mkuu wa wilaya ya Kigoma Dkt.Rashid Chuachua ameelekeza Mamlaka ya maji Kigoma kumsimamia vyema mkandarasi ili atekeleza mradi huo kwa ufanisi.
Aidha Dkt.Chuachua amemataka mkandarasi kukamilisha kazi kwa wakati ili adha wanayokabili wananchi wa maeneo hayo iweze kukoma na dhima ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Kumtua mama ndoo Kichwani iweze kutimia.
Akitoa taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) Ndugu Poas Kilangi amesema mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha miezi 12 ambapo Kuwasa itakuwa ikimsimamia mkandarasi katika Kipindi chote hicho.
Kilangi ameongezea kwa kusema utekeleza wa mradi huo ni hatua endelevu za serikali za kuboresha huduma ya maji huku kupitia ujenzi wake utawezesha (KUWASA) kufikia asilimia 95 kama ambavyo ilani ya (CCM) inaelekeza ambapo kwa sasa hali ya utoaji wa huduma ya maji kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji na kata mbili za Halmashauri ya Kigoma ni asilimia 92.
Wakizungumza kwa niaba ya Wananchi madiwani wa kata za Mwanga kaskazini Shaloni Mshanya na Diwani kata ya Buhanda Kilahumba Ruturi maeneo mbayo ni wanufaika wa mradi huo wametia pongeza za dhati kwa Mkurugenzi (KUWASA) kwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi lakini pia kupongeza serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza Miradi.