National News

JOJO ZATUMIKA KAMA MBADALA WA CHENJI STENDI

Tarehe: 14 Nov, 2024


#KIGOMA:Madiwani wa Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma,wamelalamikia kuhusiana na suala la Wananchi kupewa Jojo kama sehemu ya Chenji pale wanapotoa kiasi cha zaidi ya Shilingi 200 iliyopangwa Kama sehemu ya kiingilio katika stendi ya Mabasi Masanga iliyopo kigoma Mjini.

Hoja hiyo imeibuliwa na Diwani Ramadhani Yusuph, katika kikao cha robo Tatu ya Mwaka cha Madiwani ya Manispaa hiyo, ambapo amesema kuwa wanapokea malalamiko kutoka kwa Wananchi ikidaiwa kuwa watoza ushuru stendi ya Masanga Manispaa ya Kigoma Ujiji wamelifanya zoezi la kugawa Jojo kama mbadala wa chenji.

”Haya malalamiko unayosema ni sahihi yapo lakini pia ukiangalia kupata shilingi mia ni changamoto,inawezekana hiyo ni staili ya kujiongeza basi mtu asiache hela halafu hakutafuna hata Jojo…basi apewe hata jojo basi amejiongeza huyo mtu sasa tukubaliane”. Amesema Yusuph.

Akijibu hoja hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa Afisa Mipango Manispaa ya Kigoma Ujiji Julias Ndele amesema jambo hilo halikubaliki huku akiwataka wanaofanya vitendo hivyo kuacha maramoja.

“Katika malipo yote halali lazima stakabadhi itolewe inayoendana na malipo uliyoyafanya kwahiyo kama amelipa shilingi miatano akarudishiwa miambili na kupewa jojo, je stakabadhi aliyopewa ilikuwa inasoma kiasi gani hicho ndiyo cha msingi hili halikubaliki na tutachukua hatua kuanzia hivi tunavyoongea wale wote wananofanya pale Mwekahazina naomba wapate taarifa hii na waache maramoja mtindo huo na yeyote atakayefanyiwa hivyo basi ni vema atuletee uthibitisho huo” alisema Ndele. 

Katika hatua nyingine baadhi Madiwani hao wameshauri kutumia sheria ndogo inayowaruhusu kubadili kiasi cha kiingilio hicho ili kuziba mianya ya watu kujipatia fedha nje ya utaratibu uliopangwa.