National News

KIGOMA YATEKELEZA AGIZO UGAWAJI MICHE YA MICHIKICHI

Tarehe: 06 Nov, 2024


#KIGOMA:Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dkt.Rashid Chuachua ametoa wito kwa Wananchi katika Wilaya ya Kigoma kuendelea kulima zao  Michikichi kwa wingi ikiwa ni pamoja na kupanda miche ya Kisasa ili kuendelea kupata mavuno bora zaidi na kulipa thamani zao hilo.

Dkt.Chuachua  ameyasema hayo wakati wa zoezi la ugawaji wa Miche ya Michikichi aina ya Tenera kwa wakulima katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu uzalishaji na ugawaji wa miche ya kisasa ya zao hilo ili kulipa thamani kutokana na serikali kulifanya kuwa la kimkakati.

"Serikali imeamua kulifanya Chikichi kuwa zao la kimkakati kwakuwa tuna mahitaji makubwa sana ya matumizi ya mafuta kupikia, na Serikali  inaagiza mafuta mengi kutoka nje kupitia wafanyabiashara ili tuweze kukidhi mahitaji ya ndani ya mafuta ya kupikia. Ukweli ni kwamba ni juhudi za serikali sasa za kutaka kufufua na kukuza zao la Chikichi na kwenda kutengeneza unafuu wa kuagiza bidhaa hii kutoka nje".Alieza Dkt. Chuachua.

Akisoma taarifa kwa mkuu wa Wilaya Afisa Kilimo Manispaa ya Kigoma Ujiji Paschal Bahati amesema kuwa katika agizo alilolitoa Waziri Mkuu kila Halmashauri Mkoani ilitakiwa kuzalisha Miche Milioni 1,000,000 hadi ifikapo Juni 2025 pamoja na kuigawa bure kwa Wakulima ambapo kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji, jumla ya Miche laki 360,620 imeshagawiwa kwa wakulima wa Halmashauri hiyo huku Miche 5,500 ikiwa imepandwa kandokando ya barabara za lami katika mitaa takribani 10.