National News

DIRA YA RAIS SAMIA KUIFANYA TANZANIA NAMBA MOJA UZALISHAJI CHAKULA AFRIKA

Tarehe: 31 Oct, 2024


#HABARI:Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelezea dira yake ya kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika kupitia mikakati mitatu mikuu ya Serikali katika sekta ya kilimo. 

Akiwa nchini Marekani tarehe 30 Oktoba, 2024, aliposhiriki kwenye mjadala kuhusu kilimo barani Afrika katika mji wa Des Moines, Iowa, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali yake imejizatiti kukuza sekta ya kilimo ili kufikia lengo hilo.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Samia amebainisha mikakati mitatu muhimu ya kuendeleza ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika Miundombinu ya Umwagiliaji ambapo serikali imepanga kuwekeza katika miradi mikubwa ya umwagiliaji ili kuhakikisha ardhi nyingi zaidi inakuwa na uwezo wa kuzalisha mazao kwa mwaka mzima na hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza utegemezi wa mvua.

Mkakati mwingine ni kuboresha upatikanaji wa Teknolojia na Pembejeo za Kisasa ili kuongeza tija na ubora wa mazao, ambapo serikali inashirikiana na wadau wa maendeleo kutoa teknolojia za kisasa na pembejeo kwa wakulima ambapo itasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kupata mazao bora yenye thamani kubwa kwenye masoko ya ndani na nje.

Sambamba na mipango mingine mpango wa tatu ni Kukuza Masoko ya Mazao ya Kilimo na serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanapata masoko ya ndani na nje, na hivyo kuwapa wakulima faida zaidi kutokana na juhudi zao. 

Vilevile Rais Dkt. Samia alieleza kwamba kwa mikakati hii, Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika na hivyo kuchangia zaidi kwenye usalama wa chakula katika kanda nzima.