National News

WIZARA YA UTALII YAWAPA SOMO WABUNGE

Tarehe: 31 Oct, 2024


#HABARI:Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Wabunge wenye Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) kwenye majimbo yao, lengo ikiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu malengo ya ushirikishaji jamii katika uhifadhi, faida zake, kanuni na marekebisho yake ambapo semina hiyo imefanyika jana Oktoba 30,2024 katika ukumbi wa Bunge, Jengo la Utawala jijini Dodoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wabunge wameishauri Serikali kufanya maboresho ya kanuni za (WMAs) ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mapato yanaenda moja kwa moja kwa jumuiya hizo, kuwepo kwa utaratibu maalum wa kushughulikia changamoto ya Wanyama wakali na waharibifu pamoja na kuwa na program za mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS).

Pia wamependekeza kuendelea kuwepo kwa chombo cha kuunganisha jumuiya hizo ili ziweze kuwa na chombo cha kuwasemea kuhusu masuala yanayohusu uendelezaji na usimamizi wa (WMAs).

Akizungumza baada ya semina hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewashukuru wabunge hao kwa mapendekezo ya kuboresha jumuiya hizo ambazo ni msaada katika kuendeleza uhifadhi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb), Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara/Vitengo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.