#AFYA:Wahitimu wa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo katika program ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na dharura wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kuokoa maisha ya wagonjwa hao wanaowategemea wakati wa dharura.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa mahafali ya kwanza ya program hiyo inayofanywa na JKCI kwakushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dkt. Kisenge alisema program hiyo ya miezi sita imekuwa ikifanywa na JKCI kipindi cha nyuma hadi hapo ndoto ya kushirikiana na UDSM ilivyotimia ambapo wahitimu hao wamekuwa wahitimu wakwanza kumaliza mafunzo hayo tangu ushirikiano huo ulivyoanza mwezi machi mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Tafiti Prof. Nelson Boniface alisema JKCI inatekeleza jukumu la UDSM la kuendeleza maaarifa na mafunzo kwa kufanya tafiti na kutoa ujuzi kwa wataalamu wa afya.
Prof. Nelson aliwataka wahitimu hao kuishukuru JKCI kwa kutoa fursa kwao kuweza kupata ujuzi na kupewa nafasi ya kutumia vifaa tiba vya kisasa wakati wa mfunzo kwa vitendo.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wamesema kuwa baada ya kukutana na wauguzi kutoka nchini Zambia na kubadilishana nao ujuzi ameiona Tanzania kuwa na uwezo mkubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa mahututi na wadharura uwezo ambao wauguzi wakipitia mafunzo hayo wanaweza kufanya kazi nchi yoyote.