#HABARI:Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaanza zoezi la kunadi vitalu 24 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia mwezi Machi 2025 katika kipindi cha Kongamano na Maonesho ya Mafuta na Gesi Asilia Afrika Mashariki yatakayofanyika nchini.
Kapinga amesema hayo wakati akihutubia Kongamano la Wiki ya Mafuta Afrika linalofanyika nchini Afrika Kusini ambalo limehudhuriwa na washiriki kutoka nchi 70 duniani kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu mafuta na gesi asilia.
Vilevile amesema katika duru la tano la kunadi vitalu vya gesi asilia, Wizara ya Nishati imejipanga kuvitangaza vitalu vyote 24 ambapo visima 21 vipo Bahari ya Hindi na vingine vipo ziwa Tanganyika.
Aidha ameeleza kuwa, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zilianza miaka ya 1950 ambapo hadi sasa kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa ni takriban futi za ujazo Trilioni 57.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, amesema hiyo ni ajenda ya nchi na kinara wake ni Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anashirikiana na wadau wengine kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafikiwa.
Kupitia mkutano huo, Mhe. Kapinga ameeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini kupitia Wizara ya Nishati pamoja na kuwaalika wawekezaji kuwekeza nchini.
Amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Kuhusu sekta ya umeme, Kapinga amebainisha miradi inayofanyika nchini kwa ajili ya kuimarisha gridi ya Taifa, ikiwemo mradi wa umeme Jua Kishapu, mradi wa Julius Nyerere utakaozalisha megawati 2,115 pamoja na miradi mingine ikiwemo ya upepo ili kuhakikisha gridi inaimarika.