#HABARI:Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ya asilimia 50 ya bei kwa mitungi ya gesi inayosambazwa nchini na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 10, 2024 na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Christina Mndeme wakati wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo 2024 yanayofanyika katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro.
Amesema kuwa, lengo ni kupunguza gharama kubwa ya nishati hiyo na kila Mtanzania aweze kuimudu gharama ya kuipata nishati safi ya kupikia.
"Rais Samia ni kinara wa nishati safi nchini na ndiye anayetuhamasisha kuendelea kutumia nishati safi sisi watanzania kwa kutoa ruzuku ya bei kwa kila mtungi wa gesi hii," Amesema Mndeme.
Vile vile, Mkuu wa wilaya ya Gairo Jabir Makame ameipongeza (REA) kwa kuendelea kugawa mitungi ya gesi na majiko banifu kwa wananchi wa wilaya hiyo na kusisitiza elimu kuendelea kutolewa kwa matumizi sahihi ya nishati hiyo.
Kwa upande wake, Mhandisi Deusdedit Malulu ametoa elimu ya nishati safi ya kupikia, umuhimu wa nishati hiyo, madhara ya matumizi ya nishati chafuzi na namna bora ya matumizi ya teknolojia ya nishati safi.
"Nimetoa elimu ya namna bora ya kutumia teknolojia ya nishati bora ya kupikia pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na (REA) katika miradi ya nishati safi ya kupikia, " Amesema.
Hadi sasa jumla ya kampuni nne zimepewa dhabuni na (REA) ya kusambaza gesi ikiweno Taifa gas ili kusambaza mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.