VIJANA JITOKEZENI KUJIANDIKISHA DAFTRI LA MPIGA KURA
Tarehe: 07 Oct, 2024
#DAR ES SALAAM:Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo, ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024, ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, amewataka vijana pia kuchangamkia fursa za kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kigamboni, Bw. Erasto Kiwale, ambaye pia ni msimamizi mkuu wa uchaguzi katika manispaa hiyo, amewahakikishia wananchi kuwa maandalizi yote kuelekea uchaguzi yamekamilika, ikiwemo utoaji wa matangazo kwenye ngazi mbalimbali. Aidha, ameeleza kuwa vituo vya kujiandikisha vitakuwa kwenye majengo ya umma yaliyotengwa maalum kwa ajili ya mchakato huo.
Bw. Kiwale pia ameweka bayana tofauti kati ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na orodha ya wapiga kura wa Serikali za Mitaa hivyo akiwataka wananchi kutambua umuhimu wa kushiriki katika michakato yote miwili.
Pia, amesisitiza kuwa hata wale wenye vitambulisho vya zamani vya wapiga kura wanapaswa kujiorodhesha tena kwa ajili ya uchaguzi huu wa mitaa.
Mwenyekiti wa Jogingi, Bw. Silaji Ramadhani, ameshukuru kwa kutambuliwa na Mkuu wa Wilaya na ameahidi kushirikiana na vijana wa Kigamboni katika kuhamasisha wananchi kujiandikisha. Pia ameeleza kuwa wapo tayari kupita kila kata kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi huu.
Taarifa zaidi kuhusu mchakato wa kujiandikisha zitapatikana kwenye mitandao ya kijamii ya Kigamboni na kupitia matangazo rasmi ya Serikali.