National News

AMANI,UTULIVU VYAWAVUTA WEWEKEZAJI TANZANIA

Tarehe: 30 Sep, 2024


#UWEKEZAJI:Uwepo wa amani na utulivu, ukuaji wa kasi wa uchumi, na uwepo wa rasilimali nyingi na za kutosha nchini Tanzania, Wawekezaji wengi wa bara la Afrika hususani taifa la Nigeria wanatarajiwa kumiminika kwa wingi kuja kuwekeza nchini hapa.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Binilith Mahenge wakati alipokutokana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FIT Group ya Nigeria, Chief Loretta Aniagolu.

Kupitia ziara yake iliyofanyika mwezi Juni, 2024, kwenye Kongamano la Uwekezaji kati ya Nigeria na Tanzania Dkt. Mahenge amesema walitumia Kongamano hilo kuwaeleza wenyeji fursa nyingi za uwekezaji zilizopo nchini hapa.

Vilevile, Dkt. Mahenge amesema ana imani na nchi za Afrika kujitosheleza na uwepo wa mitaji ya kutosha ya uwekezaji, hivyo ana imani ya kuwa Tanzania inaendelea kupata Wawekezaji wengi kutoka bara la Afrika na si mataifa ya Ulaya na mabara mengine pekee.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FIT Group Chief Loretta Aniagolu amethibitisha kuwa Tanzania ni mahala salama pa uwekezaji kwa nchi za Afrika Mashariki na kwamba Loretta amesema atashawishi Menejimenti na Bodi ya Kampuni hiyo kukamilisha uwekezaji wao kwenye sekta ya Majengo ya Biashara.

Aidha, amesema ataenda kuzishawishi Kampuni za nchini Nigeria kuja Tanzania kufanya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali, kwa sababu ukiwekeza Tanzania, una uhakika wa kupata usaidizi wa karibu kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC).