National News

TANESCO WAHIMIZWA KUONGEZA KASI USIMAMAIZI WA MRADI WA UMEME

Tarehe: 19 Sep, 2024


#KIGOMA:Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko amesema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu Mkoa wa Kigoma utakuwa umeunganishwa kwenye gridi ya taifa na kuachana na matumizi ya mejenereta katika uzalishaji wa Umeme Kigoma mjini na mkoa mzima kwa ujumla.

Dkt.Biteko ameyasema hayo leo tarehe 19 Septemba,2024 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kituo cha kusambaza umeme msongo wa Kilovoti 400/220/132/33 Kidahwe wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma huku  akitoa wito kwa wakandarasi na (TANESCO) kuongeza juhudi katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwanufaisha Wananchi wa Kigoma na maeneo jirani.

”Na hivi tunavyozungumza mwenyekiti wetu wa kamati ya kudumu ya Bunge alivyosema kwamba ni lini tutapata umeme wa gridi ya taifa hapa Kigoma? Nadhani swali hilo Joyce Ndalichako, Mbunge wa Buhigwe, Kakonko na Kibondo wasingeweza kuliuliza kwasababu wapo kwenye gridi, lakini bahati mbaya wapo kwenye gridi ya umeme mdogo wenye msongo wa Kilovoti 33 ambao nao watakuelezea matatizo wanayokutana nayo, hapa Kigoma nataka nielekeze tena kama ambavyo viongozi wetu wameshakwisha kusema mwisho mpaka tunapomaliza mwaka huu tuzime tena Majeneta hapa Kigoma Mjini, Kigoma iunganishwe na gridi ya Taifa” amesema Dkt.Biteko.

Aidha Dkt.Biteko amesema kuwa katika Jimbo la Kigoma Kaskazini lenye jumla ya Vijiji 46, Vijiji 41 vimeunganishwa na Umeme ambapo katika Vijiji hivyo kuna jumla ya vitongoji 182, Vitongoji 157 tayari vimeunganishwa na Umeme huku vitongoji 75 vilivyosalia Wakandarasi wakiendelea na kazi ya kuunganisha umeme.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa mkoa wa Kigoma unaenda kuwa hazina ya umeme nchini kutokana na kupokea umeme kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo kutoka chanzo cha Umeme wa maji mto Malagarasi hadi Kidahwe na kutoka Katavi kwa msongo wa Kv 400 pamoja na laini ua umemewa SGR kutoka Dar Es Salaam wenye Kv 220.

Awali akitoa salamu mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa Mkoa huo katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umepokea kiasi cha shilingi Trilioni 11 na Bilioni 500 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo Barabara,maboresho ya kiwanja cha ndege na umeme huku akiahidi kusimamia miradi yote inayotekelezwa mkoani hapa.