MAFUNDI MIFUMO YA UMEME WAPIGWA MSASA KUHUSU LESENI
Tarehe: 17 Sep, 2024
#HABARI:Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt John Mboya, amewasihi mafundi umeme wote mkoani humo kuhakikisha wanakuwa na leseni za ufungaji mifumo ya umeme zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa mujibu wa Kifungu cha. 8 (h) cha Sheria ya Umeme,Sura Na. 131.
Dkt.Mboya ameyasema hayo wakati akifungua Semina ya siku moja kwa niaba ya mkuu wa huo Thobias Chacha ambapo amesema kuwa wamepiga vita mafundi vishoka, na kwamba anaamini kwamba baada ya semina hiyo kila asiye na leseni ataomba leseni ili afanye kazi kwa uhalali.
Vilevile amewasihi wasipoteze fursa hiyo kwani mkoa huo una miradi mingi ambayo ni fursa kwa mafundi umeme na kuongeza kuwa sasa vishoka wote hawatapewa kazi mpaka pale watakapokuwa na leseni ya EWURA.
Meneja wa (EWURA) Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher, amesema semina hiyo iliyowashirikisha mafundi umeme na wadau zaidi ya 150, ililenga kuwajengea uwezo wataalam na wadau hao kuhusu sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa utendaji kwenye shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme.
Wadau wengine walioshiriki semina hiyo ni Wakala wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).@ewura