SERIKALI YATOA RUZUKU MITUNGI YA GESI ZAIDI YA 400,000
Tarehe: 13 Sep, 2024
#NISHATI:Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, amesema Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa na unafuu katika upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ikiwemo mitungi ya gesi ili kumwezesha kila mwananchi kutumia nishati iliyo safi na salama.
Katika kutekeleza jitihada hizo, Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya awali ambayo inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara huku zoezi hilo likiwa ni endelevu.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 13 Septemba 2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya Kusainiwa mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na taasisi sita ambazo ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Jeshi la Magereza (TPS) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia, hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.
“Namshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yanayowezesha Sekta ya Nishati kuendeshwa kwa mafanikio ambayo yamepelekea leo hii tushuhudie hatua ikizidi kupigwa katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuokoa maisha ya watanzania na pia kuiwezesha Wizara ya Nishati kutatua changamoto zinazojitokeza lengo likiwa ni kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.” Amesema Dkt. Biteko
Kuhusu mikataba hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia, Dkt.Biteko ameiagiza REA na wadau kuhakikisha kuwa matokeo yanaonekana tena kwa uharaka akieleza kuwa “itakuwa aibu sana watanzania wanaona mikataba imesainiwa huku kukiwa hakuna matokeo, tusione kawaida kwa ndugu zetu kupoteza maisha kwa kutumia nishati isiyo safi, tuwaokoe kupitia miradi hii na tutumie kila fursa inayojitokeza.” Ameleeza Dkt.Biteko.
Akizungumzia jengo la REA alilolizindua, Dkt.Biteko amesema litawawezesha watumishi kutoa huduma kwa wananchi na kuwapongeza REA kwa kujenga jengo hilo la kisasa lenye ghorofa tano kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8 kwa miezi 18 badala ya shilingi bilioni 13 zilizopangwa awali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa majengo ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake yanafungwa mfumo wa umeme jua ikiwa ni kuonesha kwa vitendo matumizi ya nishati safi yenye gharama nafuu.
kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema tukio hilo ni alama ya ushirikiano kati ya (REA) na Taasisi za Jeshi ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti wa rasilimali za misitu na kutengeneza fursa za ajira kupitia Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) kuwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 ziache matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia vyanzo vya Nishati safi ya Kupikia ikwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa.
Amesema kwa sasa nishati inayotumika kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu ni kuni kwa asilimia 98 ambapo Jeshi hilo lilianza kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza kutumia nishati safi kupitia gesi asilia na mkaa mbadala hivyo kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha Jeshi la Magereza kutumia nishati safi ya kupikia kwenye magereza yake.
Amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itahakikisha fedha zilizotengwa pamoja vifaa kwenye programu hiyo zinasimamiwa ipasavyo ili lengo tarajiwa lifikiwe na hii ikienda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa Jeshi ili waweze kuisimamia na kutunza miundombinu itakayofungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa pongezi kwa REA kwa kukamilisha jengo kubwa la kisasa ambalo linaifaharisha Dodoma na pia amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh.bilioni 214 kwa ajili ya shughuli za umeme mijini na vijijini ambapo mkoani Dodoma asilimia 92.2 ya vijiji vimefikiwa na umeme huku kazi hiyo usambazaji umeme ikiendelea.
Pia amempongeza Rais, kwa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia uhamasishaji wa nishati hiyo na kueleza kuwa kasi ya kutumia nishati safi kwa wananchi inaongezeka.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizindua mjadala wa kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia na kutilia mkazo wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwamba Wizara ya Nishati ina wajibu wa kutekeleza agizo hilo na ndio maana taasisi yake ya REA imesaini mikataba husika
Amesema Mikataba iliyosainiwa inahusisha masuala mbalimbali ikiwemo kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na usambazaji wa majiko na mitungi ya gesi ipatayo laki nne ambayo inatolewa kwa bei ya ruzuku kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisema kuwa, Wakala huo kuhamia kwenye jengo lake kumewezesha kuokoa shilingi milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo ya huduma zinazotolewa.
Kuhusu mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza, mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57 zitatolewa na (REA) na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi hilo kwa mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 ya Tanzania Bara.